2. Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu

Mbuga ya Gasi Valafu ilipendwa sana na kundi la wanyama wenye miguu minne sababu ya uwepo wa maji meupe, katika lugha yao “Gasi Valafu”.

Mwaka mmoja ikatokea kwamba, baada ya kukosa kunyesha mvua ya kutosha, wanyama wote wakaanza kuhangahika sana kupata maji ya kunywa. Hali mbaya zaidi ikawa kwa watoto wao wadogo.

Mwaka uliofuata, mvua ikakosa kabisa kunyesha. Uhaba mkubwa ukaingia katika mbuga ya Gasivalafu.

Ndipo wanyama wakaamua uitishwe mkutano ili kujadili tatizo hilo kubwa ajabu: sharti maji yapatikane kwa njia moja au nyingine. Wakaamua kuchimba kisima kireeefu mpaka maji yapatikane. Ikapangwa siku ya kuanza kazi na ratiba ya kazi ingeendelea hadi kupata maji.

Wanyama weeengi wakajitahidi kujitokeza katika kazi hiyo ya kufa na kupona. Majina yao yakaandikwa na mwandalizi kwa mtindo wa kunyofoa manyoya na kuyahifadhi katika kibuyu cha siri. Kazi ikaendelea siku hadi siku bila hata kupumzika.

Sungura tu hakuhudhuria hata siku moja, akifikiri fikiri moyoni mwake: “Nikiulizwa kwa nini sishiriki kazi hiyo muhimu kwa jumuiya, nitajitetea na kusema kuwa nafanya kazi kila siku, lakini msimamizi wa kazi huwa hanioni sababu mimi ni mdogo kuliko wanyama wengine”. Kumbe sungura asijue kuwa kuliwekwa msimamizi wa kufuatilia mahudhurio katika kazi, hilo hakulijua kabisa!

Kazi ikawa nyingi, jasho kibao na mwishowe maji yakapatikana: meupe, tena metameta na ya baridi. Habari ya mafanikio ya kazi zikaenea mpaka hata sungura akasikia sifa ya hayo maji.

Kumbe!! Hatimaye ukombozi ukafika kwa wanyama.

Lakini kikabaki bado kitu kimoja cha kutekeleza, jinsi ulivyokuwa mpango toka awali: kulinda kisima na kuhakikisha kuwa maji yanachotwa na waliofanya kazi tu. Wanyama wengine wasisogee wala wasijaribu kuyachota, la sivyo wangeshtakiwa na kupata adhabu kubwa ajabu. Sungura naye akawekwa katika mabano: Je! akija kuchota maji itakuwaje?

Kumbe! Sungura akawa anaendelea kuyachota maji ya kisima kipya kwa mpango wake wa siri.

Nao wanyama wenzake waliofanya kazi kwa upande wao wakawa wanaendelea kufanya uchunguzi kwa siri. Ikafika siku: ikagundulika kuwa makanyagio yaliyopatikana jirani na kisima yalikuwa ya Bwana Sungura. Mara ukawekwa ulinzi mkali.

Sungura naye akawa anatumia ujanja wake akidamka alfajiri na mapema kuchota maji ili asionane na wengine. Bahati mbaya siku moja akakamatwa akiwa ndani ya kisima, akawekwa chini ya ulinzi. Lakini akafaulu, akakurupuka, akakimbia. Akaendelea kuyachota maji kwa ujanja wake siku hadi siku.

Akabadilishwa mlinzi mwangalifu zaidi, na sungura akakamatwa tena. Sungura akatumia ujanja mwingine. Akamwambia mlinzi abamizwe kwenye vumbi, hapo bila shaka ataumia vibaya sana. Akafanyiwa kama alivyoomba na mara akamtimulia vumbi mlinzi na kukimbia mbio.

Akawekwa mlinzi mwingine mwerevu zaidi. Huyo akamtengenezea ulimbo akaufunika kwa kitambaa, ikawa kama mtu amelala. Sungura akafika tena kuchota maji, akaona kama mlinzi amelala, akaanza kumtukana aliyelala, asipate jibu lolote. Mwishowe akasogea na kutaka kumpiga mlinzi, akafanya hivyo. Kumbe akanata pale pale na kukamatwa mara moja. Akashtakiwa kwenye Baraza la wazee, akapewa adhabu ya kupigwa viboko kila siku asubuhi.

Hivyo ndivyo vilivyomsababisha sungura kukosa kukua, akawa mfupi na kuendelea kujificha katika majani hadi hii leo.

Na: Kat. Romanus Luhanga

Nessun commento: