7. Kwaresima na ukatekumeni

Kwenye makala zilipopita tulisoma kwamba tafakari ya Kipindi cha Kwaresima cha Mwaka A inahusu Ubatizo. Tena kiistoria kipindi hicho kilikuwa cha pekee kwa mafundisho ya mwisho ya wakatekumeni wabatizwa siku ya Pasaka. Mafundisho yalitolewa hasa kutokana na masomo ya kila Dominika.

Katika Parokia yetu, utaratibu wa Ukatekumeni ni mojawapo kati ya mipango muhimu ya kichungaji. Basi tuangalie kwa kifupi machache yaliyo muhimu kuhusu Ukatekumeni.


a. Mifano iliyotumika kuelezea Ukatekumeni.

Tangu karne za kwanza za Kanisa, mifano kadhaa ilitumika ili kueleza maana ya ukatekumeni, nayo ni:

* Mfano wa “Urekuruti wa kijeshi”: anayetaka kuwa mwanajesi, atakuwa kwanza “rekuruti”, yaani anapewa mafunzo ya msingi tena mazito, ndipo anatoa kiapo cha kuitumikia nchi yake kwa nguvu zake zote. Msingi wa mfano huo ni maneno ya Mtume Paulo anayemfananisha mkristu na askari:

Piga vita vile vizuri vya imani, shika uzima ule wa milele ulioitiwa, ukaungama maungamo mazuri mbele ya mashahidi wengi (1Tim. 6: 12).

Taz. pia: 2Kor. 10:4; 1Tim. 1:18; 2Tim. 4:7.

* Mfano wa kibiblia: dhamira ya "Kutoka": Maisha ya kikristu yalifananishwa na safari ya Waisraeli jangwani: inaanza siku ya ubatizo (ni kama kuvuka bahari ya Sham) na kuendelea mpaka kufikia nchi ya ahadi (mbinguni). Mfano huo umetumika kwa kutilia mkazo kwamba Ukatekumeni ni muda wa kujizoesha kuishi kufuatana na Neno la Mungu linalomwongoza mtu.

* Mfano wa “kubeba mimba”: Msingi wake ni kulitazama Kanisa kama mama. Kuzaa hakufanyiki kwa siku moja tu, bali huchukua muda mrefu: kutunga mimba, kubeba mimba kwa miezi tisa na mwishoni kuzaliwa kwa mtoto. Kufanywa mkatekumeni ndio kutungwa kwa mimba tumboni mwa Mama Kanisa. Ukatekumeni ndio muda wa kubeba Mimba. Ubatizo ndiyo kuzaliwa (mara ya pili) katika uzima wa ki-Mungu:

Taz.: 1 Petro 1:23: "Maana kwa njia ya neno hai la Mungu, neno la milele, ninyi mmezaliwa upya, si kama watoto wa baba awezaye kufa, bali baba asiyekufa milele."


b. Dikrii juu ya kazi za kimisioni za Kanisa (Ad Gentes) na hati nyingine za Kanisa

Dikrii hiyo iliyotolewa na Mtaguso Mkuu wa Vatikano wa II mwaka 1965, katika ibara 13 - 14, inaeleza kinagaubwaga nia ya Kanisa kuhusu Ukatekumeni, ambao ni:

* safari ya kiroho, yenye ibada zake

* kuacha hali fulani ya maisha na kuingia katika hali nyingine,

* mabadiliko katika mawazo, mwenendo, tabia,

* malezi ya jumuiya nzima ya wakristu wa mahali,

* malezi yanayoendelea katika maisha yote,

* ni unyago wa kweli wa kikristu

“Mtu anapoingizwa katika ukatekumeni, lazima aingizwe kwa ibada (liturjia) rasmi, kwani huo si muda wa kupewa mafundisho tu, bali ni unyago wa kweli wa kikristo wanapoundwa katika mai-sha yote ya kikristu. Ndiyo maana jambo hilo lazima liwe linafanwa hatua kwa hatua ama kwa ibada takatifu zinazofululiza baada ya muda maalum hasa wakati wa kwaresima. Na ubatizo utolewe siku ya ibada za Pasaka. Jumuiya nzi-ma ya waamini inapaswa kushiriki katika kuwa-ingiza wakatekumeni katika ukristu ili tangu mwanzo wakatekumeni wajione wamekuwa se-hemu ya Taifa la Mungu. Juu ya hayo wajione wameingia katika Jumba la Mungu na wameisha anza kuishi maisha ya imani, matumaini na mapendo.” (Ibara 14)


Katika hati nyingine za Kanisa na pia Katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki, zinaelezwa kwa kirefu njia mbalimbali ambazo inafaa kuzitumia ili wakatekumeni wakomae kiimani. Kwa kifupi njia hizo ni:

* Katekesi: kumwelewesha wakatekumeni fumbo la wokovu. Njia hiyo huwaingiza katika imani.

* Mazoezi ya Kikristo, yanayomwezesha mkatekumeni kusali na kumwomba Mungu, kuelewa liturjia, kudhihirisha imani katika mazingira anamoishi, kumtegemea Kristo katika yote, kushika na kuwajibika katika sheria ya Mungu, hasa amri ya upendo, kujikana mwenyewe.

* Ibada mbalimbali, zinazowasaidia wakatekumeni watakaswe.


c. Utaratibu wa Ukatekumeni jinsi ulivyo.

Kwa kifupi ndivyo ulivyo utaratibu wake:

* Kipindi cha Watakaji: ni muda ambapo anayetaka au anayeshauriwa kuwa mkristo, anajiandikisha kwa katekista, ndipo pamoja na waombaji wengine anaanza kupata elimu ya kikristo hasa ikilinganishwa na mazuri ya mazingira yake. Ibada fupi inafanyika kwa kuwatambulisha kwa wakristo.

* Kipindi cha Uanafunzi (au Kuhubiriwa Habari Nje-ma): mafundisho ya kipindi hicho yatahusu kuhubiriwa Habari Njema yaani ufunuo wa Mungu kwetu katika Agano la Kale, na tangazo linalomhusu Mwokozi wetu Yesu Kristo, yaani Agano Jipya. Mwishoni mwa kipindi hicho ipo ibada ya pekee, ndiyo hatua inayowafanya wanafunzi wawe wakatekumeni, na kupokelewa kanisani rasmi.

* Kipindi cha Ukatekumeni: mafundisho ya kipindi hicho ndiyo Katekisimu na katekesi inayomwezesha mkatekumeni kuelewa kwa undani kabisa fumbo la wokovu na kuanza kuyatekeleza. Isiwe tu elimu ya kujua au kujifunza inavyofanyika, kwa mfano, mashuleni. Ibada au hatua itakayofanyika ni Ibada ya Uteuzi, inayowaingiza katika kipindi kinachofuata.

* Kipindi cha Uteuzi (au kutakaswa na kuangazwa): madhumuni yake ni matayarisho ya pekee yana-yohusu sakramenti za kiingilio. Kipindi hiki huangukia katika majira ya pekee, yaani Kwaresima na Paska. Ibada ya kipindi hicho inahusu Matakaso makuu matatu na Mausia mawili (Kanuni ya Imani na Baba yetu) ambayo hukamilisha matayarisho ya kiroho kwa wateuliwa. Ni kutakasa moyo na roho, kujikinga na vishawishi, kuokoa nia na kuwasha utashi. Ibada inayofanyika mwishoni mwa kipindi hicho ni kuadhimisha sakramenti za Ibatizo na Komunio ya kwanza.

* Kipindi cha wakristo wapya (au Mistagojia): toka Pasaka hadi Pentekoste. Kinahusu mafundisho juu ya Kanisa, Sakramenti kwa ujumla na miito. Pia wanaelimishwa kuwa kuanzia sasa wanashirikishwa ufalme, unabii na ukuhani wa Kristu. Ni wakristo wenye haki na pia wajibu zote katika Kanisa.

Nessun commento: