Visualizzazione post con etichetta Z4. Hadithi. Mostra tutti i post
Visualizzazione post con etichetta Z4. Hadithi. Mostra tutti i post

2. Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu

Mbuga ya Gasi Valafu ilipendwa sana na kundi la wanyama wenye miguu minne sababu ya uwepo wa maji meupe, katika lugha yao “Gasi Valafu”.

Mwaka mmoja ikatokea kwamba, baada ya kukosa kunyesha mvua ya kutosha, wanyama wote wakaanza kuhangahika sana kupata maji ya kunywa. Hali mbaya zaidi ikawa kwa watoto wao wadogo.

Mwaka uliofuata, mvua ikakosa kabisa kunyesha. Uhaba mkubwa ukaingia katika mbuga ya Gasivalafu.

Ndipo wanyama wakaamua uitishwe mkutano ili kujadili tatizo hilo kubwa ajabu: sharti maji yapatikane kwa njia moja au nyingine. Wakaamua kuchimba kisima kireeefu mpaka maji yapatikane. Ikapangwa siku ya kuanza kazi na ratiba ya kazi ingeendelea hadi kupata maji.

Wanyama weeengi wakajitahidi kujitokeza katika kazi hiyo ya kufa na kupona. Majina yao yakaandikwa na mwandalizi kwa mtindo wa kunyofoa manyoya na kuyahifadhi katika kibuyu cha siri. Kazi ikaendelea siku hadi siku bila hata kupumzika.

Sungura tu hakuhudhuria hata siku moja, akifikiri fikiri moyoni mwake: “Nikiulizwa kwa nini sishiriki kazi hiyo muhimu kwa jumuiya, nitajitetea na kusema kuwa nafanya kazi kila siku, lakini msimamizi wa kazi huwa hanioni sababu mimi ni mdogo kuliko wanyama wengine”. Kumbe sungura asijue kuwa kuliwekwa msimamizi wa kufuatilia mahudhurio katika kazi, hilo hakulijua kabisa!

Kazi ikawa nyingi, jasho kibao na mwishowe maji yakapatikana: meupe, tena metameta na ya baridi. Habari ya mafanikio ya kazi zikaenea mpaka hata sungura akasikia sifa ya hayo maji.

Kumbe!! Hatimaye ukombozi ukafika kwa wanyama.

Lakini kikabaki bado kitu kimoja cha kutekeleza, jinsi ulivyokuwa mpango toka awali: kulinda kisima na kuhakikisha kuwa maji yanachotwa na waliofanya kazi tu. Wanyama wengine wasisogee wala wasijaribu kuyachota, la sivyo wangeshtakiwa na kupata adhabu kubwa ajabu. Sungura naye akawekwa katika mabano: Je! akija kuchota maji itakuwaje?

Kumbe! Sungura akawa anaendelea kuyachota maji ya kisima kipya kwa mpango wake wa siri.

Nao wanyama wenzake waliofanya kazi kwa upande wao wakawa wanaendelea kufanya uchunguzi kwa siri. Ikafika siku: ikagundulika kuwa makanyagio yaliyopatikana jirani na kisima yalikuwa ya Bwana Sungura. Mara ukawekwa ulinzi mkali.

Sungura naye akawa anatumia ujanja wake akidamka alfajiri na mapema kuchota maji ili asionane na wengine. Bahati mbaya siku moja akakamatwa akiwa ndani ya kisima, akawekwa chini ya ulinzi. Lakini akafaulu, akakurupuka, akakimbia. Akaendelea kuyachota maji kwa ujanja wake siku hadi siku.

Akabadilishwa mlinzi mwangalifu zaidi, na sungura akakamatwa tena. Sungura akatumia ujanja mwingine. Akamwambia mlinzi abamizwe kwenye vumbi, hapo bila shaka ataumia vibaya sana. Akafanyiwa kama alivyoomba na mara akamtimulia vumbi mlinzi na kukimbia mbio.

Akawekwa mlinzi mwingine mwerevu zaidi. Huyo akamtengenezea ulimbo akaufunika kwa kitambaa, ikawa kama mtu amelala. Sungura akafika tena kuchota maji, akaona kama mlinzi amelala, akaanza kumtukana aliyelala, asipate jibu lolote. Mwishowe akasogea na kutaka kumpiga mlinzi, akafanya hivyo. Kumbe akanata pale pale na kukamatwa mara moja. Akashtakiwa kwenye Baraza la wazee, akapewa adhabu ya kupigwa viboko kila siku asubuhi.

Hivyo ndivyo vilivyomsababisha sungura kukosa kukua, akawa mfupi na kuendelea kujificha katika majani hadi hii leo.

Na: Kat. Romanus Luhanga

1. Tatizo mwenye mkia mrefu

Hapo zamani za kale, ulikuwepo urafiki mkubwa kati ya tembo na nyani, wote walikuwa wakicheza pamoja bila ubaguzi wowote kati yao.
Ilitokea kwamba mama nyani alimzaa mtoto mwenye mkia mrefu ajabu. Alimpa jina Tatizo.
Tatizo aliendelea akakua,. na vile vile mkia wake ukawa unarefuka zaidi na zaidi. Kila siku na kila mahali ikambidi kuwa makini mkia wake usimletee shida yoyote hasa akiwa pamoja na tembo: wasiukanyage.
Kwa upande wao, nyani wenzake waliona mkia mrefu namna hiyo kama kichekesho: kila mara walipokutana naye walikuwa wakimcheka.

Siku moja katika michezo yake, Tatizo alinaswa kwenye mti kiasi kwamba hakuweza kujiokoa. Kumbe na wenzake wakamwona katika hali hiyo ngumu ajabu wakamwacha pale pale na kwenda zao kucheza sehemu nyingine. Naye Tatizo alihuzunika sana kana kwamba hata machozi yalimtoka kwa wingi: alishindwa la kufanya na tena alikosa kwenda kucheza na wenzake. Muda si muda, rafiki yake tembo, jina lake Hekima, akawa anapitia njia ile ile alisikia yowe, aliangalia juu, akamwona Tatizo amenaswa, akamsaidia akamwokoa na kurudi wote wawili pamoja nyumbani huku wakichezacheza.



Mawazo yake Tatizo yaliwa mazito na ya huzuni aliwaza sana jinsi rafiki zake walivyomkimbia bila kumsaidia wakati wa shida, kiasi kwamba jioni alishindwa kula na hata kupata usingizi.
Asubuhi yake aliamka angali amechoka, akaoga akanywa chai akaona nyani wenzake wakipita kwenda kucheza, asiwe na hamu hata kidogo ya kujiunga nao kutokana na walivyomtendea. Kwa bahati akapita Hekima, akamsalimia rafiki yake, akamshawishi asiwaze mno yaliyopita, akamshauri asijitenge na rafiki zake, aendelee kushirikiana nao katika michezo.
Tatizo akafikirifikiri, na mwishowe akapokea ushauri wa Hekima.
“Lakini, nifanye nini ili wenzangu wasione aibu sababu nimerudi pamoja nao tena baada ya kile walichonitendea?” akawaza moyoni mwake.
Alipata wazo la kucheza na mkia wake mrefu ili kuwafurahisha nyani wenzake na kuwavutia wacheze tena pamoja naye. Alianza mara moja.

Mara hii akawa kiongozi wa kwaya akitumia mkia wake kuwaongoza wanakwaya na kuimba mwenyewe. Mara ile mkia wake ukawa filimbi na muziki nzuri ikasikika. Mara hii akawa mwana sarakasi na mkia wake ulimbeba akiwa hewani juu. Mara ile mkia wake ukawa mkono na kutaka kuwasalimia wenzake waliokuwa wakiangalia wakiwa bado mbali na wenye wasiwasi.
Muda si muda nyani wenzake waliacha michezo yao wakaanza kusogelea pale Tatizo alipokuwa anaendelea na mazoezi yake. Walivutwa mno na michezo yake mpaka walijikuta wote wanamshangilia mwenzao.

Aibu zao zikatoweka, wakamkaribisha Tatizo awe tena mwana kundi mwenzao.
Toka siku hiyo, wote kwa pamoja wakaendelea kucheza pamoja, kutembea pamoja na mara nyingine kula pamoja wakikaribishana nyumbani.
Lakini ... matatizo hayana mwisho!

Ilitokea kwamba siku nyingine nyani mwingine akirukaruka toka mti hadi mti, alikosea, alinaswa naye vibaya mno, alishindwa kujinasua. Wakaja majirani wengi waliaribu kila njia wasiweze kumsaidia huku kelele na vilio vikaanza sikika toka mbali.
Naye Tatizo alikimbia mbio kuona kuna nini. Alipanda haraka mpaka juu kabisa ya ule mti aliponaswa mwenzake, akamtelemshia mkia wake aliyenaswa ili aweze kuushika. Akafaulu kumwokoa na kumweka mahali pa usalama.

Wengine wote walimshangilia Tatizo kwa ujasiri wake wa kufaulu kumwokoa aliyejinasa.
Wakarudi wote nyumbani, moyo ukajaa furaha. Toka silu ile waliusahau kabisa upungufu aliokuwa nao Tatizo: wakajifunza kuwa kila mmoja ana uwezo wa kuchangia furaha ya wote.