6. Kwaresima: mpango wa liturjia

Tukiangalia Misale ya waumini tunaona kwamba Dominika za Kwaresima zina masomo ya “Mwaka A”, “Mwaka B” na “Mwaka C”. Maana yake ni kwamba masomo yanatofautiana katika miaka mitatu, kila mwaka yakilenga mada muhimu. Ila, masomo ya Jumatano ya Majivu ni yale yale kila mwaka. Kwa hiyo:

Mwaka A (mwaka 2008): wakristo wote hutafakari Sakramenti ya ubatizo. Masomo ya Mwaha A ni yale yale yaliyokuwepo tangu karne za kwanza kwa ajili ya mafundisho ya mwisho kwa wakatekumeni.

Mwaka B (mwaka 2009): wakristo wote hutafakari juu ya Kristo na juu ya Agano kati ya Mungu na watu. Mungu alifanya Agano na binadamu toka zamani za kale na Agano hilo lilitimizwa kwa njia ya Kristo aliyejitoa kwa ajili ya wokovu wa wanadamu mpaka kufa na kufufuka.

Mwaka C (mwaka 2010): wakristo wote hutafakari juu ya toba. Ni katekesi ihusuyo upatanisho na Mungu pamoja na wenzetu, ambao kilele chake ni siku ya Pasaka.

Tuangalie kwa kifupi liturjia ya Kwaresima ya mwaka huu, 2008, ambao ni Mwaka A:


Jumatano ya Majivu:

Mungu anatuomba tufanye toba:

* Toba iwe ya ndani, ya moyoni (Yoheli 2: 12-14)

* Zipo njia tatu zinazotusaidia katika kutubu kwetu, nazo ni: Kufunga, Sadaka na Sala. Hayo yatendeke si kwa ajili ya kuonekana na watu, bali kwa kukutana na Mungu tunayemhitaji katika maisha yetu. (Mathayo, 6:1-6;16-18)

Dominika ya kwanza:

Ubatizo unatupatia neema ya kuyashinda majaribu yote, kama alivyoyashinda Yesu.

* Dhambi ya asili lilitokana na kishawishi cha kuwa sawa na Mungu, yaani kiburi (Mwa., 2: 7-9; 3:1-7)

* Akimwiga Kristo, kila mkristo atafaulu kuvishinda vishawishi vikubwa anavyopambana navyo (Mt. 4: 1-11) yaani: kishawishi cha kumwona Mungu kama mtumishi wangu (mawe yawe mikate); kishawishi cha kumjaribu Mungu (jitupe chini), na kishawishi cha ubwana (hayo yote nitakupa).

Dominika ya pili:

Ubatizo ni Sakramenti inayotupatia imani na kutufanya wana wa Mungu.

* Abrahamu (Mwanzo, 12:1-4) tunamwita Baba wa imani: alipoitwa na Mungu aliacha yote kwa kumwamini yeye. Vivyo hivyo Ubatizo unatufanya tuondoke kuelekea anapotuonesha Mungu.

* Tunapoelekea ni pale tunapomwona Yesu jinsi alivyo, yaani Mungu (Enjili: Mt. 17: 1-9). Tena tunaambiwa “Msikieni yeye”.

Dominika ya tatu:

Wakatekumeni na wakristo wakimwamini Yesu na kumsikiliza, wapo tayari kuyapokea maji ya uzima toka kwake

* Waisraeli katika safari yao ya kutoka utumwani Misri kuelekea nchi ya ahadi, walimnung’unikia Mungu wakiwa na wasiwasi kuwa Mungu atawaletea maji huko jangwani (Kutoka, 17: 3-7)

* Yesu, kama alivyomwambia mwanamke msamaria kwamba anayo maji yaliyo hai, vile vile anamkaribisha mkatekumeni na kila aliyebatizwa anywe maji haya ili asione kiu tena (Yoh. 4: 5-42).

* Maji haya ni Roho Mtakatifu (Warumi, 5: 1-2, 5-8)

Dominika ya nne:
Wakatekumeni na wakristo kwa njia ya Ubatizo:

* wanatoka gizani na kupata nuru ili waangaziwe na Yesu aliye mwanga wetu (Yoh. 9: 1-41, Kipofu toka kuzaliwa).

* wanawezeshwa kuwa wana wa nuru na kuishi ipasavyo (Waefeso, 5: 8-14)

* mafuta yanawafanya waungane na Kristo aliye mfalme wetu (1 Samweli, 16: 1b, 6-7, 10-13)

Dominika ya tano:

Kwa njia ya Ubatizo:

* tunaunganika na uzima wake Kristo usiokoma ijapo miili yetu inakufa. Yeye ndiye uzima wa milele (Yohane, 11: 1-45).

* tunapata uwezo wa kumpendeza Mungu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu (Warumi, 8:8-11)



Liturjia ya Kwaresima na Ibada ya Ubatizo:

Tukiangalia mpangilio wa Dominika za Kwaresima na Ibada ya Sakramenti ya Ubatizo, tunatambua kuwa yaliyo kwenye Neno ka Mungu la kila Dominika mengine yao yapo pia kwenye Ubatizo:

Dominika ya kwanza:

* Neno la Mungu: Shetani anamjaribu Yesu, lakini Yesu anakataa.

* Katika Ibada ya Ubatizo: “Mwamkataa Shetani? Na mambo yake yote? Na fahari zake zote?”

Dominika ya pili:

* Neno la Mungu latukumbusha kuwa Abrahamu alimtegemea Mungu na kumwamini kupita yote. Tena, Yesu alipogeuka sura, “sauti ikatoka katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye”.

* Katika Ibada ya Ubatizo: “Mwasadiki kwa Mungu...? Mwasadiki kwa Yesu Kristo...?”

Dominika ya tatu:

* Neno la Mungu, katika Enjili latuambia: “Walakini yeyote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele”

* Katika Ibada ya Ubatizo: Sala ya kubariki maji yatakayotumika katika Ubatizo: “Upende kuyabariki maji haya watakayobatizwa watumishi wako. Umewaita waoshwe kwa maji haya ya kuwapatia uzima mpya katika imani ya Kanisa, ili wapate uzima wa milele”.

Dominika ya nne:

* Neno la Mungu, katika Enjili latufundisha kuwa Yesu ndiye mwenye uwezo wa kufanya Kipofu aone tena, apate kuwa mwana wa nuru.

* Katika Ibada ya Ubatizo: “Pokea mwanga wa Kristo” mzazi akikabidhiwa mshumaa uliowaka.

Dominika ya tano:

* Neno la Mungu, latuambia kuwa Yesu kabla hajamfufua Lazaro, anamwambia Martha: “Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminie mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! unayasadiki hayo? Akamwambia, Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu”.

* Katika Ibada ya Ubatizo: “Mwasadiki kwa Yesu Kristo... akafufuka katika wafu...?” Tena ishara ya msalaba katika paji la uso kwa kila mtoto.

Nessun commento: