3. Jina la “Makambako”

Jina “Makambako” lina historia ndefu.

Historia yake yaenda ndani zaidi hata kufikia vita vilivyokuwa vikipiganiwa kati ya Wangoni na Wahehe na kumalizikia kwa kila mmoja kujigamba na kushika mikono na kusema, “Sisi wote ni kambako kweli! Wote tu madume wa vita! Tu watane! Tukae kwa amani.”

Lakini maana halisi ya “Makambako” si hii, bali ni uoto wa mti mmoja tu ulioota mahali pale. Mmea huu ulikua taratibu na kufikia kuwa mti mkubwa sana.


Mti huu haukuwa mrefu sana, ila shina lake lilikuwa nene na kubwa sana.

Likapewa jina la jiti “Mpembeja”.

Watu wa mraba kama mzee Kukye walikuwa wanne na kushikana mikono waliweza kulizunguka jiti lile la mpembeja. Hakuna mti mwingine wa aina ile ulioonekana kuota chini yake au kuonekana maeneo mengine, ila huu tu.

Watu wote (mababu wetu) waliuheshimu sana mti huo. Hakuna kulima chini yake, wala kukata matawi yake hadi leo.

Ni katika eneo la jiti hilo matambiko makuu yalifanyika, na mojawapo la matambiko hayo ni lile la ukame. Kulangalangewa huanzwa mahali hapo kuendelea kulangalanga sehemu zingine maalum kama kule Kitisi na Ilangamoto. Aidha, viongozi wa Serikali,kabla ya kuvunjwa tawala za asili, mikutano ilikuwa ikiendeshwa chini ya jiti hili kuu la Mpembeja.


Hatima, jiti hili Mpembeja lilikauka. Mizizi ikaoza na likaanguka chini. Watu hawakuokota kuni wala kulipasua. Likabaki kama lilivyo na ukubwa wake.

Ndani ya gogo hili kukaoza na kutokea kama pango. Nyuki waliweza kutengeneza asali mle ndani na watu wakafaidi.

Pia kilikuwa kificho kwa watoto wakati wa jua kali na mvua pia.

Usemi ukajitokeza kwa watu, “Ee, tazameni kambako hilo! Kweli ni kambako! Hata ukimpelekea Myembi wako dume kama kambako hili la mpembeja atakusifu sana kuwa binti yangu kaolewa kwa watu wenye heshima”. Kwa kadiri watu walivyoendelea kuliongelea siku kwa siku “Kambako, Kambako”, likazaliwa jina hili maarufu la “Makambako”.

Basi, Makambako, chanzo chake chatokana na jiti la mpembeja na vita vya Wahehe na Wangoni ni vipambizo tu vya jina halisi la Makambako.

Mbegu zake ndizo zilizoota na kushtawisha enzi za jiti Mpembeja asilia.

Laiti kama Serikali ingepaweka hadhi mahali hapo pangekuwa kivutio kizuri mno kwa watalii na hivyo kuingiza fedha nchini mwetu!

Na: M.M. Kayombo


1 commento:

Anonimo ha detto...

Took me time to read the whole article, the article is great but the comments bring more brainstorm ideas, thanks.

- Johnson