Ulanzi

Ulanzi ni kinywaji kinachotokana na mmea ambao huota kwa wingi sehemu moja na hukua sana kwenda juu. Mimea hii ikiwa bado michanga hukatwa juu na ikishakatwa hutoa maji na kitu mithili ya povu hujaa juu ya pale palipokatwa. Maji hayo yanayotoka hukingwa kwenye kitu kiitwacho “mbeta”: halina kiswahili sahihi. Maji hayo yanayotoka ni matamu sana na tena yana uwezo wa kulewesha.

Historia yake.

Inasemekana ulanzi uligunduliwa na mnyama mdogo aitwaye panya ambaye kwa mara ya kwanza waling’ata ule mmea mchanga wa ulanzi na maji yakaanza kutoka. Kila siku panya walionekana kupenda kulamba ile sehemu walioing’ata. Binadamu, baada ya kugundua hilo, walifuatilia na wakajaribu kulamba na wao, ndipo walipogundua kuwa yale maji yaliyotoka ni matamu.

Basi wakakata ile mimea michanga ya mianzi na kuona maji mengi yakitoka na kitu mithili ya povu juu yake.

Baadaye wakatumia mianzi iliyokomaa kwa kutengenezea kitu cha kukingia yale maji yanayotoka. Zinaitwa “mbeta”

Maelezo

Ulanzi ni kinywaji cha asili kinachopendwa sana na watu wa mikoa ya Iringa, Mbeya na Songea, Kanda za Juu ya nchi ya Tanzania.

Ni kinywaji cha asili ambacho hakitengenezwi bali kinatokana na mti unaoitwa mwanzi.

Ulanzi unagemwa mara tatu kwa siku:

¨ Asubuhi: hugema na kutoa ulanzi kutoka kwenye vile vyombo vya kukingia (mbeta). Ulanzi huu wa asubuhi daima ni mtamu na togwa sana.

¨ Mchana huenda kugema kusudi kuweza kutoa sehemu iliyokauka ili ulanzi uendelee kutoka.

¨ Jioni: hugemwa tena na kutoa ulanzi uliomo kwenye vyombo vya kukingia. Ulanzi huu wa jioni ni mkali kidogo kwa sababu unakuwa umewakiwa na jua.

Ili kupata ulanzi ulio mzuri, wagemaji huchanganya ulanzi wa asubuhi na wa jioni ili uwe bora zaidi na kwa hiyo upendwe na wengi zaidi.

Utomvu:

Ni kitu kama uji unaotuama juu ya ile sehemu iliyokatwa kwenye kitindi kichanga kwa ajili ya kutoa ulanzi.

Kitindi

Ni mti ule unaotoa ulanzi. Kitindi ni umoja, vikiwa vingi huitwa vitindi na daima huwa vingi ili kupata vitindi vichanga vingi. Kitindi kikiwa kimoja huwezi kugema ulanzi kwa sababu kitindi kichanga hakiwezi kupatikana.

Hugemwa lini?

Ulanzi huu hugemwa kwa kipindi, kwa sehemu zilizo nyingi hasa kipindi cha kifuku (masika) ulanzi huwa mwingi sana na unazidi kupungua kadiri kipindi cha masika kinavyoisha. Lakini kuna baadhi ya sehemu ambazo zina baridi sana na hali ya ubichi kwa mwaka mzima, kwa mfano katika mbuga ya Kitulo, wilaya ya Makete (Tanzania).

Hunyweka kwa siku ngapi?

Ulanzi hunyweka kwa siku moja kimsingi hapo huwa mtamu wa ladha safi. Lakini ukishalala, ulanzi hupoteza ubora wake na hivi hauwi mtamu sana. Lakini ukichanganya na uliogemwa siku hiyo, hurudi katika hali njema tena, ingawa siyo safi sana.



Vitindi vilivyovikwa “mbeta” tayari kwa kukinga ulanzi



“Mbeta” iliyofunikwa na jani la mmea ili nyuki na ndege mbalimbali wasimalize ulanzi.



“Mbeta” iliyojaa ulanzi unaotoa povu. Ndio ulanzi unaogemwa asubuhi.



Kitindi chenye “mbeta” mbili. Pembeni, upande wa kushoto, unaona kitindi kichanga kilichokatwa na kuandaliwa tayari kwa kuvikwa “mbeta”



Binti huyu anakata sehemu ya kitindi iliyokauka ili ulanzi uweze kuendelea kutoka. Kazi hiyo hufanyika mchana.



Huyu mama anarudi nyumbani akijitwisha vipande vya mianzi vitakavyotengenezwa kuwa “mbeta”



Ulanzi uliogemwa na kuchujwa vizuri sasa unapelekwa mjini kwa kuuzwa. Siku hizi unaweka ukaona Fuso zinazobeba na kujaaa maguduria ya ulanzi.

Nessun commento: