1. Utambulisho


M
akambako
ni mji mdogo ulioko kwenye kanda ya juu, kusini mwa Tanzania, Wilaya ya Njombe na Mkoa wa Iringa. Unakaa mita 1650 hivi juu ya usawa wa bahari.

Ni mji “mchangamfu” ulioko kwenye barabara kuu inayotoka Dar es Salaam na kuelekea mpaka Zambia kupitia mji wa Mbeya. Kwa upande mwingine ipo njia panda ya barabara kuu ielekeayo kusini mwa nchi, Mkoa wa Ruvuma.

Tena ni stesheni kubwa ya TAZARA (Tanzania Zambia Railway), ambayo inatoka Dar es Salaam na kuenda mpaka Lusaka, Zambia. Ilijengwa miaka ya sitini na sabini ya karne iliyopita.

Tukiangalia sensa ya watu iliyofanyika mwa 2002, tunasoma kuwa wakazi wake mwaka ule walikuwa 52.000 hivi. Bila shaka siku hizi watu wameongezeka kiasi kikubwa na wataendelea kuongezeka kutokana na hali ya kipekee ya mji huo. Makambako ni mji wa biashara ambako watu toka pande zote za nchi wanavutwa kuishi huku ili kufanya biashara zao.

Kwa upande wa elimu, zipo Shule 13 za Msingi ambapo mwaka jana, 2006, wanafunzi wake kwa ujumla walikuwa zaidi ya 14.000. Shule za sekondari zipo 4, na kati yao moja mpaka kidato cha 6. Nyingine imeanza kidato cha kwanza mwaka huu, 2007, na nyingine imeanza kujengwa.

Kwa upande wa dini, mjini Makambako unaweza ukakuta Dini ya Kikristo (hasa Wakatoliki, Waluteri na Waanglikana), Dini ya Kiislam na Dini ya jadi.

Kwa upande wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Makambako ni mojawapo kati ya Parokia 31 za Jimbo la Njombe. Licha ya mji, parokia ya Makambako ina vigango 21.

Ilianzishwa rasmi Mei moshi 1954 na Shirika la Wamisionari wa Consolata waliokuwa katika Jimbo la Tosamaganga (kwa sasa Jimbo la Iringa). Ndio Wamisionari hao ambao mpaka sasa wanaendelea kuhudumia parokia hiyo. Mwaka huu 2007 mapadre wanaofanya kazi ya uchungaji Makambako ni hawa wafuatao: P. Igino Lumetti, toka Italy; P. Remo Villa (Paroko), toka Italy; P. Jude Katende, anayetoka Kenya na P. Marcelo De Losa, anayetoka Arjentina. Wapo pia Watawa wa kike wanaosaidia katika shughuli za kichungaji na nyinginezo: nao wanatoka Shirika la Mtakatifu Agnes, Chipole (Songea), nyumba ya Mtakatifu Gertrud, Imiliwaha (Njombe).

Unakaribishwa sana kwenye web-site yetu,
tena tunakuomba uwasiliane nasi ukitumia e-mail ifuatayo: removilla at consolata.net

Nessun commento: