4. Kwaresima,Tuangalie historia yake


Wataalamu wa Liturjia wanatuambia kuwa mpangilio wa kipindi hicho cha Kwaresima jinsi ulivyo siku hizi haukuwa hivyo tokea mwanzoni mwa Kanisa. Tena wanasema kuwa ulikuwa ulijikamilisha kwa utaratibu hatua baada ya hatua, kadiri ya ongezeko la wakristo na pia kutokana na taratibu nyingine za Kanisa.
Hapo chini tutajaribu kueleza kwa kifupi jinsi kipindi hiki cha mwaka wa Kanisa kilivyoanza kuadhimishwa na kukamilishwa karne hadi karne.

a. Karne ya pili
- Kufunga siku ya Ijumaa Kuu na Jumamosi Kuu.
Wakati huo, mwanzoni kabisa mwa Kanisa, adhimisho la Pasaka linatanguliwa na siku moja au mbili za kufunga. Ila inaonekana kuwa kufunga huku si njia maalum ya kujiandaa kwa Pasaka, bali ni hatua ya pekee ya mafundisho na pia zoezi kwa wakatekumeni ambao wanabatizwa katika adhimisho la Kesha la Pasaka. Tena mfungo huo ni kwa ajili ya wakatekumeni wenyewe, na kwa mtoaji wa Sakramenti za kiingilio kwa hao wakatekumeni. Baada ya kipindi tu hata jumuiya zima ya Kanisa inaanza kufanya zoezi hilo la kufunga.

b. Karne ya tatu
- Wiki moja ya matayarisho.
Katika karne ya tatu, wanaliturjia wanatueleza kuwa huko Roma Dominika inayotangulia Pasaka inaitwa “Dominika ya Mateso”. Tena, siku ya Ijumaa na Jumatano ya wiki hii hii, hakuna Misa takatifu inayoadhimishwa.
Zoezi la kufunga chakula kwa wiki hiyo nzima katika karne hiyo, linafanyika tu katika Jumuiya au majimbo kadhaa, kwa mfano katika Kanisa la Alexandria (Misri).

c. Karne ya nne
- Wiki tatu za matayarisho.
Mwana historia aliyeishi karne ya tano aliyeitwa Sokrates, anatuhakikishia kuwa kipindi cha Kwaresima katika karne ya nne kinadumu wiki tatu tu. Tena katika liturjia ya kipindi hicho inatumika Enjili ilivyoandikwa na Yohane, kwa sababu katika kitabu hicho sehemu nyingi zinaeleza na zinahusu Pasaka inayokaribia na tena zinaeleza habari za Yesu akiwa mjini Yerusalemu.

d. Mwishoni mwa karne ya nne
- Wiki sita za matayarisho.
Kurefushwa hivi kwa matayarisho ya Pasaka kunasababishwa na utaratibu fulani unaowekwa na Kanisa kutokana na kujitokeza kwa waumini waliokosa na wenye nia ya kupatanishwa na Mungu na Kanisa pia, hasa wale waliotenda dhambi zinazojulikana na watu (public sinners). Basi Dominika ya kwanza ya kipindi hicho, hawa huanza safari yao ya toba kabla ya kupokelewa tena katika Jumuiya.
Baadaye, mwanzo wa safari yao ya toba inapangwa kuanzia Jumatano inayotangulia Dominika ya kwanza ya Kwaresima. Siku ya Alhamisi Kuu, asubuhi, mwishoni mwa safari yao ya toba, hupokelewa tena katika Jumuiya wakipata maondoleo ya dhambi.
Mwanzoni mwa safari yao hupakwa majivu na kuvalishwa nguo za kugunia ya kuvaa: iwe alama ya toba na majuto. Ioneshe nia yao ya kumwelekea Mungu zaidi.
Kipindi hicho chote che toba kwa hao “public sinners” kinadumu siku arobaini, na kikapewa jina la kilatini la “Quadragesima” , ndiyo arobaini kwa lugha hiyo.

e. Kipindi kinarefushwa zaidi: Jumatano ya majivu
(kukaribia mwishoni mwa karne ya tano)
Unapokaribia mwisho wa karne hii ya tano, pia Jumatano na Ijumaa zinazotangulia Kwaresima wa wakati huo, zinahesabiwa kama sehemu ya Kwaresima. Mpaka liturjia ya kupakwa majivu kwa wenye nia ya kujirudi huadhimishwa siku ya Jumatano hiyo inayotangulia. Muda si muda, zoezi hilo la kupakwa majivu linaanza kufanyika kwa wakristo wote.
Ni kwanzia karne hiyo pia ambapo hatua za mwisho za Ukatekumeni, zile zinazotangulia Ubatizo unaotolewa Kesha ya Pasaka, na zinazoangukia kipindi cha Kwaresima, zinapangwa kwa utaratibu maalum.
Kwa hiyo kipindi cha Kwaresima, licha ya kuwa safari ya toba kwa wale wenye nia ya kurudi katika Kanisa, kinapewa sifa nyingine: ni kipindi cha matayarisho ya mwisho kwa wakatekumeni.
Licha ya hayo, pia “wakristo wa kawaida”, yaani wale wasiokuwa katika kundi la wenye kuhitaji upatanisho na wasiokuwa wakatekumeni, huombwa wajiunge na wenzao katika safari ya toba na matayarisho kwa ubatizo, ili wenyewe pia waweze kujiandaa vizuri zaidi kwa Sikukuu ya Pasaka wakiwa na moyo mkunjufu wa kumpokea Yesu Mfufuka.

f. Wiki saba za matayarisho (Karne ya sita)
Wakati huo, wiki nzima inayotangulia Dominika ya kwanza ya Kwaresima, huanza kuingizwa kwenye matayarisho ya Pasaka, na Dominika inayoanza wiki hii huitwa Dominika ya “Quinquagesima” (toka kilatini: siku hamsini), kwa sababu ni siku ya hamsini kabla ya Pasaka.
Mwishoni mwa karne hiyo na pia wakati wa karne inayofuata kipindi cha Kwaresima kinarefushwa tena zikiingizwa Dominika mbili zaidi.
Lakini wanaliturjia husema kuwa tendo la kurefusha kiasi hicho kipindi cha pekee kama ilivyo Kwaresima, kilisababisha kupunguzwa sana maana yake.

g. Hatima
kwa kifupi tunaweza tukasema kwamba kiistoria mpango wa namna hiyo wa Kipindi cha Kwaresima uliongozwa hasa na mambo mawili:
utaratibu wa kuwapokea wale walioomba kurudi katika Kanisa. Adhimisho lake lilikuwa siku ya Alhamisi Kuu masaa ya asubuhi.
utaratibu wa Ukatekumeni. Watu wazima walioomba kujiunga na Kanisa walikuwa wanaongezeka kila mwaka, kwa hiyo ulihitajika muda maalum kwa matayarisho yao ya mwisho kabla ya Ubatizo uliokuwa unatolewa Kesha la Pasaka.

Nessun commento: