1. Tatizo mwenye mkia mrefu

Hapo zamani za kale, ulikuwepo urafiki mkubwa kati ya tembo na nyani, wote walikuwa wakicheza pamoja bila ubaguzi wowote kati yao.
Ilitokea kwamba mama nyani alimzaa mtoto mwenye mkia mrefu ajabu. Alimpa jina Tatizo.
Tatizo aliendelea akakua,. na vile vile mkia wake ukawa unarefuka zaidi na zaidi. Kila siku na kila mahali ikambidi kuwa makini mkia wake usimletee shida yoyote hasa akiwa pamoja na tembo: wasiukanyage.
Kwa upande wao, nyani wenzake waliona mkia mrefu namna hiyo kama kichekesho: kila mara walipokutana naye walikuwa wakimcheka.

Siku moja katika michezo yake, Tatizo alinaswa kwenye mti kiasi kwamba hakuweza kujiokoa. Kumbe na wenzake wakamwona katika hali hiyo ngumu ajabu wakamwacha pale pale na kwenda zao kucheza sehemu nyingine. Naye Tatizo alihuzunika sana kana kwamba hata machozi yalimtoka kwa wingi: alishindwa la kufanya na tena alikosa kwenda kucheza na wenzake. Muda si muda, rafiki yake tembo, jina lake Hekima, akawa anapitia njia ile ile alisikia yowe, aliangalia juu, akamwona Tatizo amenaswa, akamsaidia akamwokoa na kurudi wote wawili pamoja nyumbani huku wakichezacheza.Mawazo yake Tatizo yaliwa mazito na ya huzuni aliwaza sana jinsi rafiki zake walivyomkimbia bila kumsaidia wakati wa shida, kiasi kwamba jioni alishindwa kula na hata kupata usingizi.
Asubuhi yake aliamka angali amechoka, akaoga akanywa chai akaona nyani wenzake wakipita kwenda kucheza, asiwe na hamu hata kidogo ya kujiunga nao kutokana na walivyomtendea. Kwa bahati akapita Hekima, akamsalimia rafiki yake, akamshawishi asiwaze mno yaliyopita, akamshauri asijitenge na rafiki zake, aendelee kushirikiana nao katika michezo.
Tatizo akafikirifikiri, na mwishowe akapokea ushauri wa Hekima.
“Lakini, nifanye nini ili wenzangu wasione aibu sababu nimerudi pamoja nao tena baada ya kile walichonitendea?” akawaza moyoni mwake.
Alipata wazo la kucheza na mkia wake mrefu ili kuwafurahisha nyani wenzake na kuwavutia wacheze tena pamoja naye. Alianza mara moja.

Mara hii akawa kiongozi wa kwaya akitumia mkia wake kuwaongoza wanakwaya na kuimba mwenyewe. Mara ile mkia wake ukawa filimbi na muziki nzuri ikasikika. Mara hii akawa mwana sarakasi na mkia wake ulimbeba akiwa hewani juu. Mara ile mkia wake ukawa mkono na kutaka kuwasalimia wenzake waliokuwa wakiangalia wakiwa bado mbali na wenye wasiwasi.
Muda si muda nyani wenzake waliacha michezo yao wakaanza kusogelea pale Tatizo alipokuwa anaendelea na mazoezi yake. Walivutwa mno na michezo yake mpaka walijikuta wote wanamshangilia mwenzao.

Aibu zao zikatoweka, wakamkaribisha Tatizo awe tena mwana kundi mwenzao.
Toka siku hiyo, wote kwa pamoja wakaendelea kucheza pamoja, kutembea pamoja na mara nyingine kula pamoja wakikaribishana nyumbani.
Lakini ... matatizo hayana mwisho!

Ilitokea kwamba siku nyingine nyani mwingine akirukaruka toka mti hadi mti, alikosea, alinaswa naye vibaya mno, alishindwa kujinasua. Wakaja majirani wengi waliaribu kila njia wasiweze kumsaidia huku kelele na vilio vikaanza sikika toka mbali.
Naye Tatizo alikimbia mbio kuona kuna nini. Alipanda haraka mpaka juu kabisa ya ule mti aliponaswa mwenzake, akamtelemshia mkia wake aliyenaswa ili aweze kuushika. Akafaulu kumwokoa na kumweka mahali pa usalama.

Wengine wote walimshangilia Tatizo kwa ujasiri wake wa kufaulu kumwokoa aliyejinasa.
Wakarudi wote nyumbani, moyo ukajaa furaha. Toka silu ile waliusahau kabisa upungufu aliokuwa nao Tatizo: wakajifunza kuwa kila mmoja ana uwezo wa kuchangia furaha ya wote.

Nessun commento: