5. Kwaresima, utaratibu wa siku hizi

Toka karne ya sita na ya saba mpaka katikati ya karne ya ishirini, hakuna mabadiliko makubwa yanayofanyika kuhusu kipindi cha Kwaresima.

Ni wakati wa Mtaguso Mkuu wa Vatikano wa Pili, uliofunguliwa rasmi tar. 11 Oktoba 1962 na ulioendelea mpaka mwaka 1965, ambapo Mababa waliohudhuria waliona umuhimu wa kuufanyia marekebisho ya kimsingi mpango mzima wa Kipindi cha Kwaresima.

Kwa hiyo Mtaguso Mkuu huo katika Hati ihusuyo Liturjia, iliyotolewa tar. 4 Desemba, 1963, unaagiza kuwa mpango wote wa kipindi cha Kwaresima kirekebishwe ili ueleweke kwa urahisi zaidi na ulenge zaidi shabaha ya kipindi chenyewe.

Kuhusu marekebisho ya ujumla ya Mwaka wa liturjia, Hati hiyo inasema:"Mwaka wa Liturujia urekebishwe ili zihifadhiwe au ziingizwe tena desturi na taratibu za vipindi vitakatifu kadiri ya hali ya nyakati zetu. Pia maana yao ya asili ihifadhiwe ili kulisha ipasavyo uchaji wa waamini katika kuadhimisha mafumbo ya ukombozi wa Kristo, na hasa fumbo la Pasaka. Aidha, ikiwa ni lazima, marekebisho yafanywe kulingana na hali ya kila mahali kadiri ya ibara 39 na 40." (Hati ya Liturjia, “Sacrosantum Concilium”, ibara 107)

Na kuhusu kipindi cha Kwaresima Mababa wanaagiza:

1. “Maana mbili zinazofanya kipekee Kipindi cha Kwaresima, ukumbusho wa Ubatizo au matayarisho yake, na toba, zitiliwe mkazo wa pekee katika Liturujia na katekesi ya Liturujia. Nazo zinasaidia kuwaandaa waamini kuadhimisha fumbo la Pasaka, wakisikiliza mara nyingi zaidi Neno la Mungu na kujibidisha katika kusali. Kwa hiyo:

a. Mambo yote yadokezayo Ubatizo yaliyomo katika Liturujia ya Kwaresima yapewe nafasi kubwa zaidi, na pia, kama inafaa, yaingizwe tena mengine yatokanayo na mapokeo ya zamani;

b. Vivyo hivyo ifanywe kuhusu mambo ya toba. Mintarafu katekesi, juhudi ifanywe ili iweze kuingizwa rohoni mwa waamini, pamoja na matokeo ya kijamii ya dhambi, maumbile halisi ya toba yenye kuchukia dhambi kwa sababu ni kumtukana Mungu; nafasi ya Kanisa katika tendo la toba isisahauliwe kamwe, na pia sala kwa ajili ya wakosefu ihimizwe.(Hati ya Liturjia, “Sacrosantum Concilium”, ibara 109)

2. “Toba ya wakati wa Kwaresima isiwe ni tendo la ndani na la binafsi tu, bali pia lionekanalo kwa nje na katika maisha ya jamii. Matendo ya toba na kujinyima, kadiri ya uwezekano wa nyakati zetu na mahali mbalimbali, na pia kadiri ya hali ya waamini, yasisitizwe na kuhimizwa na wale wenye mamlaka, kama ilivyoelezwa katika ibara 22. Lakini tendo la kufunga chakula wakati wa Pasaka litakuwa takatifu, nalo liadhimishwe popote siku ya Ijumaa ya Mateso na Kifo cha Bwana na kuendelea, kama inawezekana, siku nzima ya Jumamosi Kuu, ili kufikia furaha na shangwe ya Dominika ya Ufufuko kwa moyo wazi na ulioinuliwa.” (Hati ya Liturjia, “Sacrosantum Concilium”, ibara 110)

Kutokana na maagizo hayo ya Mababa wa Mtaguso Mkuu, Idara ya Kansa ihusuyo Liturjia inaanza kukifanyia marekebisho Kipindi cha Kwaresima.

Kwa kifupi, marekebisho hayo:

1. yanasisitiza kwamba maana na maadhimisho ya kipindi cha Kwaresima yalenge matayarisho ya Sikukuu ya Pasaka na ya Ubatizo;

2. yanapanga muda wa kipindi hicho: kuanzia Jumatano ya Majivu hadi siku ya Alhamisi Kuu kabla ya adhimisho la Misa ya Jioni, yaani adhimisho la “Karamu ya Mwisho”.

3. Kwenye utaratibu wa zamani zilikuwepo Dominika 4 za Kwaresima na zilifuata Dominika mbili “za Mateso”. Kwa ujumla zilikuwa sita. Katika utaratibu huo mpya imeongezeka Dominika ya tano ya Kwaresima badala ya Dominika ya kwanza ya Mateso (utaratibu wa zamani). Kwa hiyo sasa Dominika ya Mateso ni moja tu, nayo ni ile inayotangulia Pasaka inayoitwa Dominika ya Matawi. Kwa mantiki hiyo, Wiki Kuu ni mwisho wa Kwaresima na lengo lake ni kuhadhimisha na kutafakari Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo kuanzia pale alipoingia kwa shangwe mjini Yerusalemu.

Ukijichukulia muda wa kujisomea sala mbalimbali na masomo ya liturjia hasa ya kila Dominika ya Kipindi hicho bila shaka utapata nafasi kubwa ya kujitajirisha kifikra na kukomaa zaidi kiimani kuhusu fumbo kuu la imani yetu: Yesu Mfufuka.

Nessun commento: