2. Kwaresima, Mwaka wa Liturjia

Hati ya Liturjia, “Sacrosantum Concilium” ya Mtaguso Mkuu wa Vatikano wa pili, inasema:
Ibara Na. 47
Mwokozi wetu, katika Karamu ya mwisho, usiku alipotolewa, aliweka sadaka ya Ekaristi ya Mwili wake na Damu yake. Alifanya hivyo ili kuendeleza Sadaka ya Msalaba siku zote mpaka atakaporudi, kusudi amwachie Bibiarusi mpendwa, yaani Kanisa, ukumbusho wa kifo chake na ufufuko wake: sakramenti ya utakatifu (sacramentum pietatis), ishara ya umoja, kifungo cha mapendo, karamu ya Pasaka “ambamo Kristo huliwa, na roho hujazwa neema, na hutolewa amana ya uzima wa milele”.
Ibara Na. 48
Kanisa anajibidisha kwa namna nyingi kusudi waamini wasihudhurie fumbo hilo la imani kama wageni au watazamaji bubu, bali waishiriki ibada takatifu kwa akili, kwa moyo na kwa matendo, wakielewa vizuri fumbo hilo kwa njia ya matendo ya kiliturujia na sala. Waamini waelimishwe katika Neno la Mungu; walishwe katika karamu ya Mwili wa Bwana; wamtolee Mungu shukrani; wakitolea hostia isiyo na doa, siyo kwa mikono ya padre tu, bali pia pamoja naye, wajifunze kujitolea wenyewe. Tena, siku kwa siku, kwa njia ya Kristo mshenga, wakamilishwe katika umoja na Mungu na kati yao, ili hatimaye Mungu awe yote katika wote.
Ibara 102:
Mama Kanisa takatifu huchukulia wajibu wake kuadhimisha kwa kumbukumbu takatifu kazi ya ukombozi ya Bwanaarusi wake aliye Mungu, katika siku zilizopangwa katika mwenendo wa mwaka mzima. Kila juma Kanisa, katika siku aliyoiita “Dominika”, yaani “Siku ya Bwana”, anaadhimisha kumbukumbu ya ufufuko wa Bwana. Kwa namna ya pekee anauadhimisha ufufuko huo pamoja na mateso yake yenye heri mara moja kwa mwaka katika Sikukuu ya Pasaka, iliyo kubwa kuliko Sherehe zote.
Katika mzunguko wa mwaka mzima, [Mama Kanisa] analikunjua fumbo la Kristo, tangu umwilisho na kuzaliwa, hadi kupaa mbinguni, mpaka siku ya Pentekoste na kungojea kwa tumaini lenye heri kurudi kwake Bwana.
Anapokumbuka namna hii mafumbo ya ukombozi, Kanisa huwafungulia waamini utajiri wa uweza na mastahili ya Bwana wake. Kwa njia hii, uwepo wa mafumbo haya unakuwapo kwa nyakati zote, ili kutoka humo waamini waweze kuchota na kujazwa neema ya wokovu.
Kwa hiyo mwaka wa liturjia si mfululizo wa mawazo au sikukuu mbalimbali, bali ni Yesu Kristo mwenyewe, tena Yesu mfufuka. Yeye alijitolea kwa ajili ya kutuletea wokovu. Na anaendelea kutuzawadia wokovu huo kwa njia ya neema ya Masakramenti mbalimbali yanayoadhimishwa katika mwendelezo wa mwaka mzima wa kiliturjia. Kwa njia hiyo, upendo wa Mungu unaolenga wokovu wa wanadamu unaonekana katika maisha ya kila siku ya Kanisa na ya ulimwengu mzima.
Hivyo basi, tunavyojua, kiini na chemchemi ya mwaka mzima wa liturjia ni fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo.
Kwa wakristo wa jumuiya za kwanza haikuwepo sikukuu nyingine za Kanisa isipokuwa ile ya Dominika: siku ya kuadhimisa Kristo mfufuka. Kwa sababu hiyo Dominika au Jumapili, tulivyozoea kutamka, ndiyo sikukuu asilia ya wakristo. Huku kuadhimisha ufufuko wake Kristo Dominika fulani na tarehe fulani rasmi kulianza karne ya pili.
Kwa hiyo mwaka mzima wa liturjia unalenga fumbo la Pasaka linaloadhimishwa kila Dominika na mara moja kwa mwaka wakati wa sikukuu ya Pasaka.
Katika mpango huu, kipindi cha Kwaresima kinakuwa muda maalum kwa kila mkristo wa kuishi kikamilifu kila mwaka fumbo la ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, akijiandaa kwa njia ya toba na utakaso.

Nessun commento: