1. Makambako - Picha chache za zamani

Tunaanza safari yetu katika intaneti tukitumia picha chache zioneshazo jinsi ilivyokuwa Makambako miaka ya sitini ya karne iliyopita. Ukilinganisha na jinsi mazingira yalivyo siku hizi, utashangaa mwenyewe!

Wakati ule, miaka arobaini iliyopita, Makambako ilikuwa kama vijiji vingine vingi vya kwetu. Barabara kuu ya kuelekea Mbeya na Malawi ilikuwa haijakarabatiwa na kuwekwa lami. Na vivyo hivyo ilikuwa kwa barabara ya kuelekea Njombe, Songea na kusini mwa Tanzania.

Tena vinjia vingi vyembamba vilikuwa vinaongoza watu toka nyumba hadi nyumba au mashambani, na si barabara ya kupitisha magari kama siku hizi.

Hapa chini unaweza ukaangalia picha chache za miaka ile pamoja na maelezo mafupi.

Picha ya kwanza:
(picha: P. Romano Motter)

Ilipigwa toka angani mnamo mwaka 1968. Inaonesha jinsi ilivyokuwa Makambako mwaka ule. Kumbe, siku hizi popote pamejaa majengo na nyumba! Barabara kubwa uionayo upande wa kushoto, ni ile iliyokuwa inaelekea kusini mwa Tanzania kwa kupitia Njombe na Songea. Barabara iliyonyooka na yenye miti mingi ni ile iliyokuwa inafika Parokiani, na ndivyo ilivyo mpaka leo hii.

Picha ya pili:
(picha: P. Romano Motter)

Ilipigwa toka angani mwaka huo huo 1968. Inaonesha barabara kuu ya kwenda kusini mwa nchi (upande wa kushoto) na kule juu, kwenye njia panda, barabara kuu inayoelekea magharibi mwa nchi mpaka Zambia, kupitia Mbeya. Barabara zote mbili hazijawekwa lami na kukarabatiwa, kazi ambayo ilifanyika mwanzoni mwa miaka ya sabini kwa ile ya kuelekea Zambia na mwanzoni mwa miaka ya themanini kwa ile inayokwenda kusini mwa nchi.

Picha ya tatu:



Ilipigwa mwaka ule ule wa 1968. Unaweza ukaona sehemu kubwa ya eneo la Parokia ya Makambako, iliyoanzishwa rasmi mwaka 1954. Majengo yanayoonekana kwenye picha, karibu yote yapo mpaka leo, ila mengine yaliongezeka miaka iliyofuata kutokana na kupanuka kwa huduma iliyokuwa inatolewa na inayotolewa mpasa hivi leo na Parokia.

Jengo kubwa lenye maumbile ya msalaba unaloliona mwanzoni hapo chini mwa picha ni Kanisa la pili la kiparokia lililokuwa linatumika miaka ile, na ambalo siku hizi halitumiki tena.

Inaonekana pia jengo la Kanisa la kwanza la Makambako, pamoja na nyumba ya Mapadre ya miaka ile. Unaweza ukaona paa zake kwenye miti ya katikati.

Zile nyumba saba zilizojengwa katika mstari, ni nyumba za Walimu wa shule ya msingi ya Makambako, iliyoanzishwa na Parokia.


Picha ya nne:
(picha: P. Giuseppe Bargetto)

Iliyopita.ni ya miaka ya hamsini ya karne. Inaonesha Paroko wa kwanza wa Parokia yetu, P. Joseph Bargetto, akiwa pamoja na watoto waliojipanga vizuri mbele ya gari la Parokia.

Katika Picha ya tano:
(picha: Sista Wamisionari wa Consolata)

Unamwona Sista mmojawapo kati ya wale waliowasili Makambako mwaka mmoja baada ya kuanzishwa kwa parokia yenyewe, yaani mwaka 1955. Jina la Sista huyu ni Sr. Dionisia Dalmasso, wa Shirika la Masista wa Consolata. Mara baada ya kufika, masista hao walianza kutoa huduma yao kwa wagonjwa, pamoja na malezi kwa akina mama na wasichana.

Nessun commento: