8. Kwaresima: Wiki Kuu, Dominika ya Matawi hadi Jumamosi Kuu

Kuanzia Dominika ya Matawi au Dominika ya Mateso, Kanisa linakaribia adhimisho la kipasaka.

Kiini chake ni adhimisho la kufa na kufufuka kwake Yesu Kristo.

Katika wiki hii Kanisa huadhimisha, hatua baada ya hatua, matukio ya siku za mwisho za Yesu hapa duniani.


a. Dominika ya Matawi au ya Mateso

Kanisa hufanya ukumbusho wa Yesu anayeingia Yerusalemu kwa shangwe.

Matendo mawili yapo kwenye adhimisho la leo:

* Yesu anaingia Yerusalemu akishangiliwa na wenyeji na wengi waliokuja mjini kwa adhimisho la Pasaka ya kiyahudi. Kushangiliwa akiketi juu ya punda, kuna maana kuwa wanamtambua Yesu kama mfalme, kwani Punda alikuwa mnyama aliyetumika na wafalme.

Kama wakrisato tunakumbuka hayo kwa tendo la maandamano ya kuelekea kanisani tukishika matawi yaliyobarikiwa.

* Lakini ufalme wake Yesu si wa namna hii walivyompokea alipoingia Yerusalemu. Katika Enjili ya leo tunakumbushwa mara moja kuwa ufalme wake unatokana na kumtii Mungu baba yake, hasa katika magumu. Ndiyo sababu inasomwa Enjili ya Mateso yake Yesu mpaka kufa. Kujitolea kwake mpaka kufa kumetuletea wokovu.


b. Siku za kwanza za Wiki Kuu

* Jumatatu, Jumanne na Jumatano ya wiki hii ni siku za mwisho za Kwaresima. Kwa kawaida huadhimisha Sakramenti ya Upatanisho: jumuiya ya waristo kwa njia hiyo huamua kwa pamoja kuishi fumbo la Pasaka kwa uthabiti zaidi.

Nasi ndivyo tunavyofanya: siku ya jumanne tunaadhimisha pamoja Sakramenti ya Kitubio kwa vijana wote, na siku ya Jumatano kwa watu wazima.

* Alhamisi Kuu asubuhi, katika Kanisa Kuu la Jimbo, huadhimishwa Misa ya Mafuta, ikiongozwa na Baba Askofu wakiwepo mapadre wote wanaofanya kazi jimboni mwake. Katika Jimbo letu na pia majimbo mengine, kutokana na ugumu wa usafiri na hivyo mapadre kushindwa kurudi maparokiani kwao kwa adhimisho la misa ya jioni, Misa hiyo ya mafuta huadhimishwa alhamisi inayotangulia Wiki Kuu.

Misa hiyo inayoongozwa na Askofu wa Jimbo, ni sikukuu ya Mapadre ambao wakiwa pamoja na Mzee wao wa Kanisa wanakumbuka Upadre wao unaotokana na Ukuhani mmoja, ule wa Kristo.

Katika Misa hiyo Askofu hubariki mafuta ya aina tatu yatakayotumika kwa masakramenti katika kila parokia ya Jimbo kwa mwaka mzima. Nayo ni:

- Mafuta ya Krisma, yenye manukato: hutumika kwa Sakramenti za Ubatizo, Kipaimara na Upadre.

- Mafuta ya Wakatekumeni: hutumika kwa Ubatizo wa watoto na kwa maadhimisho ya Hatua za Ukatekumeni.

- Mafuta ya Wagonjwa: hutumika kwa Sakra-menti ya Mpako wa wagonjwa.


c. Siku Tatu Kuu za Mateso

Kanisa huadhimisha fumbo kuu la Pasaka katika adhimisho moja kubwa na la pekee linalodumu siku tatu:

Alhamisi Kuu jioni.

Masaa ya jioni huadhimishwa misa moja tu katika kanisa la kiparokia, wakiwepo Mapadre wote. Ila katika mazingira yetu, kutokana na kuwahudumia wakristo vigangoni, Mapadre husali misa hiyo vigangoni. Ila misa zote zenye nia nyingine hukatazwa.

Katika misa hiyo hukumbushwa Karamu ya mwisho ya Yesu. Tunakumbushwa kwa jinsi Yesu alivyotupenda mpaka alijitoa mwenyewe awe sadaka ili kutupatanisha tena na Mungu. Sadaka hii ndiyo Ekaristi tunayoshe-herekea leo. Mtume Yohane, katika Enjili tuisomayo leo haelezi jinsi Yesu alivyofanya alipotuachia Sakramenti hii, waelezavyo Waenjili wengine (Taz: Mathayo, 26: 26-29; Luka, 22: 14-20; Marko, 14: 22-24), ila anatuongoza katika uelewa wa Sakramenti ya Ekaristi kama Sakramenti ya kupendana na kutumikiana alivyofanya Yesu katika tendo la kuwatawadha mitume miguu (13: 1-15).

Ni vizuri tuvikumbuke kwa kifupi vitendo vingine vya adhimisho hilo. Navyo ni:

- Inapoanza Misa, Tabernakulo ni tupu: Yesu Ekaristi amewekwa sehemu nyingine inayofaa: leo Mapadre na waumini hupokea Komunio takatifu na Sakramenti ya adhimiso la leo.

- Wakati unapoimbwa Utukufu, kengele zote hugongwa kama alama ya kumtukuza Mungu Baba wa Mkombozi wetu kabla ya kuingia kipindi cha mateso na kufa kwake Yesu.

- Baada ya Enjili na mafundisho ya Padre, katika Jumuiya nyingi kunafuata tendo la kuwatawadha miguu kwa watu kumi na wawili wakiwa kama Mitume. Linatukumbusha maana ya Ekaristi: kupendana na kutumikiana.

- Kabla ya kumaliza Misa, Sakramenti iliyobaki, itakayotumika katika Adhimisho la Ijumaa Kuu, kwa maandamano inapelekwa, sehemu palipopambwa vizuri na ambapo, baada ya Misa kuisha, wakristo wanashauriwa kubaki ili kuabudu fumbo kuu la Ekaristi.

Ijumaa Kuu

Siku hii Kanisa huadhimisha mateso na kufa kwake Yesu Kristo. Ni siku ya huzuni na ya kilio, lakini hasa wakristo hutafakari, maana ya sadaka ya Yesu: alijitolea kwa upendo mpaka kufa, lakini kufa kwake si mwisho ya yote.

Kwa kumheshimu Yesu aliyekufa, leo hakuna adhimisho la misa, wala la Sakramenti zo zote, kwa kufuata mapo-keo ya tangu zamani. Ila hufanyika adhimisho la Mateso yake, ikiwezekana sa ile ile ambapo Yesu alikufa, yaani saa 9.00 alasiri. Madhehebu yenyewe ni kama ifuatavyo:

* Liturjia ya Neno. Masomo ni kama ifuatavyo:

Somo la kwanza: (Isaya 52:13–53:12). “Mtumishi wa Bwana” atawakomboa wanadamu wote kwa njia ya mateso makali. Utabiri huu umetimia kikamilifu katika Yesu.

Somo la pili: (Waebrania, 4:14-16: 5:7-9). Yesu Kristo “kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu” alionja taabu na mateso mengi “akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii”.

Enjili: (Yohane, 18:1-19:42). Ndiyo kiini cha ibada ya leo: kutafakari na kufanya ukumbusho wa jinsi Yesu alivyowaokoa wanadamu. Yohane anamwo-nesha Yesu kama ndiye mfalme, mkubwa, ingawa anatendewa kama mjasusi wa hali ya juu. Mshindi ndiye yeye.

Sala kwa ajili ya watu wote. Ni sala kumi za kuwaombea watu wote: kanisa linatambua kuwa wokovu wa Yesu ni kwa wote.

* “Kuabudu” Msalaba Mtakatifu. Tunajua kuwa tunamwabudu Mungu peke yake. Ila leo kwa nam-na ya pekee tukiuheshimu msalaba unaotukumbusha jinsi Yesu alivyotuokoa tunamwabudu Yesu na kumshukuru kwa upendo aliotuonesha. Lazima leo Msalaba upewe nafasi ya mbele na ya pekee.

* Komunio Takatifu. Leo hakuna misa isomayo popote duniani. Kwa hiyo altare ni tupu na vitambaa vinawekwa sasa. Sadaka Kuu ni Yesu mwenyewe tunayemwadhimisha akifa msalabani. Kwa hiyo Mapadre na wakristo wote wanakomu-nika na Sakramenti iliyowekwa jana, Alhamisi Kuu.

Tukumbuke kuwa Ijumaa Kuu ni siku ya kufunga kama alama ya nje ya kushirikiana na Sadaka ya Kristo.

Jumamosi Kuu (mpaka jioni)

Siku ya leo Kanisa linakaa kwenye kaburi la Bwana wetu Yesu Kristo likitafakari mateso na kifo chake.

Hakuna adhimiso la misa takatifu, hali altare ipo tupu mpaka zitakapoanza sherehe za Pasaka kuanzia jioni kwa adhimisho la Vijilia au Kesha la Pasaka.

Kila mkristo siku ya leo huitwa “kwenda jangwani” akiwa peke yake mbele ya Mungu, akitafakari:

- utulivu unaopatikana akiishi na amani kwa Mungu,

- jinsi ya kulitegemea kabisa Neno la Mungu,

- uhakika wa kwamba ahadi zote za Mungu zimetimia sasa kwa njia ya Yesu Kristo msulibiwa.

Nessun commento: